Saturday, 29 November 2014

MFUNGJI BORA WA MABAO NCHINI KENYA ATUA DAR KIMYA KIMYA

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Daniel Muzeyi ‘Dan’ Sserunkuma yupo Dar es Salaam tangu juzi akifanya mazungumzo na klabu ya Simba SC.
Sserunkuma amefikia katika hoteli moja maarufu Kariakoo, Dar es Salaam kwa ugeni wa kimichezo, Sapphire Court na inaelezwa mazungumzo yamefikia pazuri.
Mzaliwa huyo wa Desemba 4, mwaka 1989 mjini Kampala, Uganda Mkataba wake na klabu yake ya sasa, Gor Mahia ya Kenya unaisha mapema mwezi ujao.
Pamoja na uongozi wa Gor kudai upo kwenye mazungumzo na mchezaji huyo mfupi mwenye misuli ambaye kwa Uganda anaitwa Majjid Musisi mpya, lakini sasa inagundulika yupo Dar es Salaam akifanya mpango wa kubadilisha ofisi.  Sserunkuma ni mchezaji aliyezaliwa na kukulia wilaya ya Lubega mjini Kampala na alisoma shule maarufu iliyoibua vipaji vya nyota wengi Uganda, St. Mary's ya Kitende.
Nyota kibao wanaotamba kisoka Uganda wamepita shule hiyo kama Joseph Owino, David Obua, Eric Obua, Emmanuel Okwi na Ibrahim Juma.
Pia utotoni mwake, alipitia katika akademi ya Friends of Football akiwa ana umri wa miaka 10, kabla ya kuchezea Express kuanzia 2008 hadi 2011 alipohamia Victors alikocheza hadi 2012 alipokwenda Kenya kujiunga na Nairobi City Stars hadi mwaka 2012 alipotua Gor Mahia.
Sserunkuma ni mfungaji bora mara mbili mfululizo kwa misimu miwili iliyopita ya Ligi Kuu ya Kenya, wakati pia mwaka 2012 alikuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya nchi hiyo.
Mwaka 2013, Sserunkuma alishinda tuzo ya Mchezaji Bora Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (USPA) Uganda, akiwapiku Tony Mawejje aliyekuwa anacheza Norway na mshambuliaji wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbarara (MUST), Siraje Muhindo.
Tayari Simba SC ina wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu, ambao ni Waganda, beki Joseph Owino, mshambuliaji Emmanuel Okwi, Warundi kiungo Pierre Kwizera na mshambuliaji Amisi Tambwe pamoja na Mkenya, Paul Kiongera.
Bado haijulikani Simba SC itamuacha mchezaji gani, kumsaini Sserunkuma, lakini kuna uwezekano Kwizera aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu kutoka Ivory Coast anaweza kuachwa kwa sababu hana tena nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Pamoja na hayo, Tambwe pia anaweza kuwa kwenye hatari hiyo, kwa kuwa hakubaliki mbele ya kocha Mzambia, Patrick Phiri licha ya kwamba ndiye mfungajki bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita.   

0 comments: