Klabu ya Azam FC imegoma kutoa kitita cha dau la usajili dola 15,000 (sawa na shilingi milioni 26) kwa ajili ya kumsajili kiungo wa Simba, Amri Kiemba katika usajili wa dirisha dogo msimu huu.
Kauli hiyo imekuja siku chache tangu Azam FC ilipojibiwa barua na Simba ya kumtaka kiungo huyo kwa mkopo katika usajili wa dirisha dogo msimu huu lililofunguliwa Novemba 15, mwaka huu.
Azam FC ndiyo ilianza kuandika barua ya kumuomba kwa mkopo Kiemba ikiwa ni siku chache tangu asimamishwe na uongozi wa timu hiyo pamoja na wenzake, Shaaban Kisiga na Haroun Chanongo.
Katibu Mkuu wa Simba, Stephen Ally, alisema wamepokea barua ya majibu kutoka Azam FC hivi karibuni ya kukataa kutoa kiasi hicho cha fedha huku ikisisitiza kumuomba kwa mkopo.
Stephene alisema mara baada ya kupokea barua hiyo, amepanga kupeleka suala hilo kwenye Kamati ya Utendaji ya timu hiyo ambayo itatoa majibu sahihi kuhusiana na hatma yake.
“Tunashukuru tumepokea barua ya majibu kutoka Azam FC hivi karibuni juu ya kumhitaji Kiemba katika usajili wa dirisha dogo baada ya kumuomba kutuandikia barua ya kumhitaji kwa mkopo.
“Sisi katika majibu yetu tuliwaambia hatupo tayari kumuachia kwa mkopo Kiemba na badala yake watupatie dola 15,000 za usajili ili tumuachie aende akaichezee Azam FC ambayo imeonyesha nia ya kumsajili,” alisema Stephen.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Azam FC, Said Mohamed kuzungumzia hilo, alisema: “Hatupo tayari kutoa fedha yoyote kwa ajili ya kumsajili Kiemba, sisi tulimuomba kwa mkopo mchezaji na siyo kumnunua moja kwa moja, wenyewe kama hawataki basi.”
0 comments:
Post a Comment