Tuesday, 29 October 2013

VYETI VYA KUZALIWA VYA TOLEWA MASHULENI

 
Gazeti la HabariLeo limechapisha habari ya Bi. Lucy Lyatuu ikiripoti kuwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) una mkakati wa kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio shuleni ambapo itaanza na shule za msingi za Serikali za jijini Dar es Salaam.

Meneja Masoko na Mawasiliano wa RITA, Josephat Kimaro alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana akisema kuwa kazi hiyo itafanyika katika Wilaya ya Ilala kwa kushirikiana na Idara ya Elimu ya Wilaya: “Mpango huo utaanza hivi karibuni, umeshafikia
pazuri na hiyo imetokana na mafanikio yaliyopatikana baada ya kufanya majaribio katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora.”

Alisema mkakati huo utaanzia katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam ambapo Wakala huyo atakuwa anapeleka fomu kwa walimu watakaozigawa kwa wanafunzi ambao nao watazipeleka kwa wazazi wao kwa ajili ya kujazwa.

Baada ya kugawa fomu, wasajili watahakiki na wale ambao wataonekana kuwa na sifa watarejeshewa. Alisema mpango ni kuona kuwa mpango huo baadaye unahamia katika shule za sekondari.

Mkakati huo wa kugawa vyeti shuleni una lengo la kuongeza idadi ya Watanzania waliosajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.

Aidha alisema mkakati huo pia ulifanywa kwa taasisi mbalimbali nchini na akatoa wito kwa makundi mengine yanayohitaji huduma hiyo, kutuma fomu kwa wakala huo.

Hadi sasa taasisi 42 za jijini Dar es Salaam watumishi wake walishakabidhiwa vyeti vya kuzaliwa.

“Katika huduma hiyo katika taasisi, Wakala hutoa fomu za maombi na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa katika maeneo waliyoko baada ya kupitia hatua zote stahili,” alisema Kimaro na kuzitaja taasisi zilizopatiwa vyeti kuwa ni majeshi ya Ulinzi na Usalama, Taasisi za kidini, Wizara, Makampuni na Mashirika mbalimbali.

 

0 comments: