Marais wa Sudan na Sudan Kusini
wamekubaliana kubuni mikakati ya kusuluhisha maswala yote yanayotatiza
uhusiano wa pande hizo mbili.
Viongozi hao walikutana leo wakati wa mkutano wa faragha katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba.Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit alielezea furaha yake kwa kufikia makubaliano ya pande hizo mbili akisema kuwa serikali yake itajitolea kuhakikisha kuwa makubaliano hayo yatatekelezwa.
Kwa upande wake Rais Umar al-Bashir alisema kuwa mkutano ulifanikiwa na kuongeza kuwa serikali yake itajitolea kuhakikisha kuwa makubaliano waliyoafikia yanatekelezwa.
Marais hao walifanya mkutano wa faragha muda mfupi baada ya Bashir kuwasili na wajumbe wake wa Sudan katika Ikulu ya Rais mjini Juba.
Kwa mujibu wa shirika la habari la SUNA, baadhi ya maswala yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni mambo tete kuhusu Abyei,usalama pamoja na kutekelezwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Mnamo siku ya Jumatatu, waziri wa mambo ya nje wa Sudan Kusini Barnaba Marial Benjamin, aliambia kituo cha redio cha Sudan CRN kuwa marais hao wawili watazungumzia mgogoro wa Abyei katika kutaka kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Kuhusu swala la kura ya maoni kuhusu Abyei , waziri alisema kuwa Muungano wa Afrika hauruhusu uamuzi wa pande moja kuhusu kura ya maoni.
Aliongeza kuwa Kura ya maoni lazima iruhusiwe na nchi hizo mbili na kuidhinishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Aidha alisema kuwa sudan Kusini inashurutishwa na makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na kwa hivyo haiwezi kuunga mkono kura ya maoni inayoshinikizwa na upande mmoja.
Hata hivyo alisema anaelewa kwa nini jamii ya Abyei iliamua kupiga kura ya maoni kujitenga na ni kwa sababu ya masaibu waliyoyapitia.
Alisisitiza kuwa Muungano wa Afrika na Sudan lazima ziisikilize jamii ya Abyei na kukubaliana kuhusu tarehe ya kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu kutaka kujitawala wenyewe.
0 comments:
Post a Comment