HOME »
» MSAFARA WA WAZIRI NCHIMBI WAPIGWA MAWE
|
|
MSAFARA wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel
Nchimbi, umepigwa mawe na wananchi waliojitokeza kuzungumzia kero ya
daraja la Matarawe, ambalo linadaiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya
watatu mwezi Oktoba mwaka huu.
Tukio hilo limetokea jana saa 10:00 jioni hadi saa 12:00, ambapo
wananchi hao wakiwa na hasira walifanya fujo wakimshinikiza Nchimbi
ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini awasaidie kupanua daraja
hilo ambalo kwa muda mrefu limesababisha kutokea kwa ajali za mara kwa
mara katika eneo hilo.
Wananchi hao wa Kata ya Matarawe, Manispaa ya Songea, wakiwamo
waendesha pikikipiki maarufu kwa jina la ‘yeboyebo’ walifunga
barabara kwa zaidi ya saa mbili huku wakifanya fujo za kung’oa kingo
za daraja, kuweka magogo na mawe katikati ya daraja na kuchoma matairi
moto ili kumzuia kiongozi huyo asiweze kupita na atoe majibu ya kina
juu ya daraja hilo.
Hatua hiyo ilililazimu Jeshi la Polisi kuwatawanya wananchi hao kwa
kuwafyatulia mabomu ya machozi ili kukabiliana na uharibifu pamoja na
kuruhusu msafara huo uweze kupita.
Aidha, kufuatia vurugu hizo, Jeshi la Polisi liliweza kuwashikilia watu wanane.
Hata hivyo Dk. Nchimbi alilazimika kusimama na kushuka kwenye gari
lake akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wa chama na serikali
akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Songea, Joseph Joseph Mkirikiti, ambapo
aliwapa pole kwa ajali zinazotokea huku akiwataka kuwa na subira wakati
ombi lao linashughulikiwa.
“Natoa pole sana kwa msiba na ajali ambazo zimetokea nimewasikia, na
ninaahidi nitawajengea daraja hili, kama nimeweza kujenga barabara
hii kwa kiwango cha lami bila maandamano wala kufungiwa barabara
nitashindwa daraja?” alihoji.
Nchimbi alisema kuwa vitu hivyo vinavyozungumzika hakuna haja ya
kufanya maandamano na kuwataka wananchi hao kuhudhuria mkutano wake kwa
kuwa anajua ufinyu wa daraja hilo na ameahidi kulifanyia maboresho
zaidi.
Naye Diwani wa kata hiyo, James Makene, aliungana na kundi la
wananchi hao na kumueleza Nchimbi kuwa hiyo ni changamoto ambayo
wakazi wake wamekuwa wakilia kwa kipindi kirefu.
Aidha, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Deusdedit Msimeki, alisema kuwa
kufuatia vurugu hizo tayari watu wanane wanashikiliwa na wanaendelea
kuhojiwa zaidi ili kuwabaini vinara wengine waliosababisha fujo hizo.
na Stephano Mango, Songea TANZANIA DAIMA
|
|
|
0 comments:
Post a Comment