Monday, 2 May 2016

Mamlaka ya Bandari-TPA Yataja Sababu Iliyosababisha Mizigo Bandarini Dar es Salaam Kupungua

Siku moja baada ya serikali  kuziagiza mamlaka ya Bandari-TPA, na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kufanya uchambuzi wa kina ili kubaini sababu za kupungua kwa shehena ya kontena zinazoingia nchini kupitia Bandari ya Dar es salaam kwenda nchi jirani, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Injinia Alois Matei, leo amejitokeza mbele ya waandishi wa habari  ili kutaja chanzo cha mizigo kupungua bandarini.

Agizo la kuzitaka mamlaka ya Bandari-TPA, na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kufanya uchambuzi  huo lilitolewa juzi Bungeni   April 30 na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dr. Philip Mpango .

Dr  Mpango alisema katika kipindi cha mwezi Oktoba mwaka jana na Machi mwaka huu kontena zilizopelekwa nchini Congo zilishuka kutoka 5,529 hadi 4,092, wakati yale yaliyokuwa yakipelekwa nchini Malawi yalishuka kutoka kontena 337 hadi 265, huku yale ya Zambia yakishuka kutoka 6,859 hadi kufikia 4,448, hivyo akaziagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania-TPA na Mamlaka ya Mapato-TRA, zichambue mwenendo huo ili kubaini chanzo cha kupungua.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Injinia Alois Matei amesema sababu kubwa  ya kupungua kwa makontena hayo imesababishwa  na kuyumba kwa  uchumi wa dunia  hasa China na kwingineko ambako mizigo inayopitia bandari ya Dar es Saam hutoka.

“Biashara za bandari dunia nzima zimeshuka.Kipindi hiki kuna mtikisiko kidogo kutokana na uchumi wa dunia kuyumba hasa China na kwingineko.

"Juzi tuliongea na wenzetu wa Singapore ambao walikuja hapa nchini, nchi yao ni moja ya nchi inayofanya biashara ya bandari kwa kiasi kikubwa. Wao pia walisema wamekumbana na tatizo hilo la kushuka kwa mizigo katika kipindi cha hii miezi mitatu." Amesema Matei

Katika hatua nyingine, Injinia  Matei  amesema serikali imepanga kutumia dola milioni 690 kuimarisha miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza uwezo wa kupokea mizigo hadi kufikia tani milioni 38 ifikapo 2030 kutoka tani milioni 16 za mwaka 2014/15.

Akifafanua kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Matei amesema mradi huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Benki ya Dunia,Trade Mark East Africa na DFID  na unatarajia kuanza   kabla ya mwisho wa mwaka 2016.

“Serikali,Benki ya Dunia,Trade Mark East Africa na DFID zimetiliana saini makubaliano ya ushirikiano wa utekelezaji wa mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam” alisisitiza Matei.

Akizungumazia maeneo yatakayohusika katika maboresho hayo Injinia Matei amesema kuwa yatahusisha uboreshaji na uongezaji wa kina kufikia mita 14 katika gati namba 1 hadi 7 ili kuwezesha meli kubwa zaidi kutia nanga.

Maeneo mengine ni ujenzi wa gati mpya ya kushushia magari katika eneo la Gerezani Creek, uchimbaji ili kuongeza kina cha lango la kuingilia meli hadi kufikia mita 14 pamoja na sehemu ya kugeuzia meli.

Eneo jingine  ni uhamishaji wa gati la mafuta la Koj pamoja na bomba la mafuta katika eneo la ujenzi, uboreshaji wa mtandao wa reli ndani ya bandari na ujenzi wa sehemu ya kupakilia na kushushia mizigo.
Mhandisi Mkuu  wa TPA Bi Mary Mhayaya akitoa ufafanuzi kuhusu mradi wa Flow meter mpya ya Kigamboni ambao umeshakamilika na hivyo kuwezesha mafuta yote yanayoingia  nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam kupimwa na kujulikana kiasi halisi kilichoingizwa hapa nchini ili kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki ikiwemo kodi
 

0 comments: