Monday, 2 May 2016

CAG, Msajili wa Hazina Watofautiana Kuhusu Shirika la Pride

Wakati Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) akisema Pride (Promotion of Rural Initiatives and Development Enterprises) ni shirika la umma, Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru anasema hana nyaraka zinazoonyesha shirika hilo kuwa la Serikali bali anajua kuwa ni asasi isiyo ya kiserikali (NGOs).

Kauli hiyo ya Mafuru imekuja siku chache baada ya CAG kutoa ripoti ya ukaguzi wa hesabu za mwaka 2014/ 2015 ambayo inaeleza kwamba shirika hilo la utoaji mikopo ni mali ya Serikali.

Kama ilivyo katika ripoti za mwaka 2013/ 2014, safari hii CAG amesisitiza kwamba Pride ilianzishwa Mei 5, 1993 chini ya Sheria ya Makampuni (CAP 212) kwa lengo la kutoa mikopo midogo kwa wajasiriamali.

Ripoti zote mbili za CAG zinabainisha kwamba fedha za kuanzishia taasisi hiyo zilitoka Shirika la Maendeleo la Norway (Norad) kwa makubaliano baina ya Serikali za Tanzania na Norway. Pia, Serikali ya Sweden ilijiunga kukifadhili chombo hicho mwaka 2001.

Katika ripoti ya mwaka 2014/ 2015, CAG anasema kwa mujibu wa taarifa ya Msajili wa Hazina ya uwekezaji wa Serikali katika makampuni, kufikia Juni 30, 2008 hisa zote za Pride zilikuwa zinamilikiwa na Serikali.

Lakini kuanzia siku hiyo, shirika hilo liliondolewa kwenye orodha ya mashirika ya umma.

“Uhalali na sababu za kuondolewa kwa shirika hili katika orodha ya Msajili wa Hazina hazikuweza kubainika. Kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008, kila Shirika la Umma linatakiwa kuleta hesabu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ajili ya kukaguliwa katika kipindi cha miezi mitatu baada ya kumalizika kwa mwaka wa fedha. Hata hivyo, hesabu za Pride Tanzania hazijawahi kuwasilishwa kwenye ofisi yangu kwa ajili ya ukaguzi kama inavyotakiwa na sheria,” anasema CAG.

Lakini Msajili wa Hazina, Mafuru alikuwa na maelezo tofauti na CAG.“Hatuna ‘document’ (nyaraka) yoyote inayoonyesha kuwa Pride Tanzania Ltd ni shirika la Serikali. Kama ulivyosema kwenye taarifa hiyo ya CAG, taasisi hiyo ilianzishwa kwa sheria ya makampuni inayosimamiwa na Brela (Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni),”alisema Mafuru.

“Serikali inaweza kuanzisha kampuni kwa kuhamisha mtaji; mlipaji ambaye ni Serikali atapeleka kiasi cha fedha kwa shirika lililoanzishwa cha Sh100 bilioni kupitia Benki ya Uwekezaji nchini (TIB).

“Kuna mashirika yanayoanzishwa kwa matamko ya Serikali kama vile Brela, Ewura (Wakala wa Udhibiti wa Nishati na Maji), TCRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania). Kuna mashirika yanayoanzishwa kwa Sheria za Bunge, nayo yanakuwa ya umma.

"Lakini Serikali haikuweka mtaji Pride wala haikutamka, ndiyo maana kwenye ofisi hii (Msajili wa Hazina) hakuna kumbukumbu yoyote.”

Msajili huyo alisema inawezekana Serikali iliidhamini taasisi hiyo wakati Norad ilipotoa mtaji kipindi cha kuanzishwa kwake.

“Sababu ya Pride kupitia Serikali, inawezekana Norad hawakuwa na uhakika na sekta binafsi. Serikali ilikuwa kama msimamizi tu, lakini haina hisa,” alisema Mafuru.

Mkurugenzi mkuu wa Pride yenye makao yake jijini Arusha, Rashid Malima alisema Msajili wa Hazina ndiye mwenye majibu sahihi.

Malima alisema Pride Tanzania ilindikishwa mwaka 1999 chini ya sheria ya makampuni (Cap 1,2) ikiwa ni kampuni ambayo iko chini ya wadhamini isiyokuwa na hisa.

“Sheria inatoa nafasi kwa anayetaka kuandikisha kampuni kuangalia ni aina gani ya kampuni anayotaka kuandikisha na inafuata sheria ipi ya uandikishwaji wake. Pride Tanzania iko chini ya wadhamini ambao kimsingi sheria inazuia wao kuwa wanufaikaji tofauti na kampuni yenye hisa ambayo wahusika ni wanufaikaji,” alisema Malima.

Huku akinukuu ripoti ya CAG, Malima alisema mwaka 2008 ilikuwa taasisi ya Serikali. lakini 2010 inaonyesha iliondolewa na CAG hana maelezo ya kutosha kwanini haipo chini ya kampuni za Serikali zinazopaswa kukaguliwa na ofisi yake.

“Kimsingi makampuni yote yanasajiliwa na Msajili wa Hazina na ndiye mwenye kufahamu kwa usahihi hatua zote za taasisi au kampuni iliyokuwa ya Serikali kuwa ya binafsi,” alieleza.

Kuhusu nani huwa anakagua hesabu zao, Malima alisema huwa zinakaguliwa na taasisi ya kimataifa ya Ernst & Young.

Mwenye jukumu la kukagua hesabu za Serikali pamoja na mashirika ya umma ni CAG, lakini kutokana na ukubwa wa jukumu hilo huwa anateua mashirika kama Ernst & Young au Deloitte et Touche. 

Akijibu maswali bungeni mjini Dodoma Machi 30 mwaka jana kuhusu hadhi ya Pride, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima alisema taasisi hiyo si ya kiserikali.

“Mheshimiwa Spika, taasisi ya Pride Tanzania ni asasi isiyo ya kiserikali iliyosajiliwa kama kampuni tarehe 5 Mei, 1993 chini ya wadhamini wasio na hisa (Company Limited by Guarantee, Not Having Share Capital), kulingana na Sheria ya Makampuni Cap, 212 ya mwaka 2012, ” alisema Malima.

“Lengo la kuanzishwa kwa asasi hiyo ni kuwawezesha walengwa wake kiuchumi kwa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati sehemu za mijini na vijijini.

"Asasi hii ina mtandao wa jumla ya matawi 71 katika mikoa yote na baadhi ya wilaya za Tanzania Bara na Zanzibar.”

Alikuwa akijibu bungeni swali la Amina Mwidau aliyetaka kujua sababu za Pride kupotea kwenye orodha ya taasisi za serikali ambayo iliiwekea dhamana wakati ikianzishwa.

0 comments: