Wednesday, 1 April 2015

Rais wa Shirikisho la Soka Kenya achafuka kwa rushwa


Kenya
Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Sam Nyamweya, amechafuka kutokana na jina lake kuwamo kwenye orodha ya watu wanaojihusisha na rushwa nchini humo iliyotolewa leo na Baraza la Maadili na Kuzuia Rushwa (EACC) akihusishwa na utafunaji wa ovyo wa fedha za shirikisho hilo.
Kwa mujibu wa mitandao ya michezo ya Kenya leo, Nyamweya amekamata nafasi ya 92 kwenye orodha ya viongozi ‘wachafu’ kutokana na kujihusisha na rushwa nchini Kenya huku ikielezwa kuwa kesi yake inachunguzwa.
Alhamisi ya wiki iliyopita, yaani Machi 26, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, aliwataka viongozi wote walioingia kwenye orodha hiyo kukaa pembeni kupisha uchunguzi na tayari viongozi mbalimbali nchini humo wakiwamo Makatibu wa Baraza la Mawaziri, wameshaachia ngazi.
Kinachosubiriwa kwa sasa nchini Kenya ni kuona Nyamweya ambaye amekuwa kiongozi wa juu ya shirikisho hilo tangu 2011, akiacha kazi.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya FKF wamekaririwa wakisema Nyamweya anapambana kuhakikisha anachuguliwa tena kuliongoza shirikisho hilo katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

0 comments: