Wednesday, 1 April 2015

MWANDOSYA AOMBWA KUGOMBEA URAISI NA VIONGOZI WA SHIRIKISHO LA VYUO VIKUU MBEYA.


 Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyuo vikuu Mkoa wa Mbeya(CCM),Raymond Mweli akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) wakikanusha kuhusu wenzao kutumia jina la shirikisho hilo kumshawishi Mwandosya kugombea urais
 Katibu Shirikisho la Vyuo vikuu Mkoa wa Mbeya(CCM),Karimu Nyanga akisoma tamko kuhusu wenzao kutumia jina la shirikisho hilo kumshawishi Mwandosya kugombea urais.
 Baadhi ya viongozi wa Shirikisho wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.
 Baadhi ya Waandishi wa habari wakichukua maelezo kutoka kwa viongozi wa shirikisho.

SHIRIKISHO la Wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoani Mbeya limeonekana kuwa na mkanganyiko juu ya tamko lililotolewa na baadhi ya wanashirikisho hilo la kumtaka mbunge wa Rungwe Mashariki Prof.Mark Mwandosya kugombea urais.
Mkanganyiko huo umekuja baada ya matamko mawili kutolewa kwa siku tofauti na wanashirikisho hilo,moja likimtaka Prof Mwandosya kuchukua fomu na jingine likilaani tamko la awali kuwa lilikuwa batili.
Tamko lililotolewa  na katibu wa jumuiya hiyo Karimu Nyanga kwa wanahabari lilibainisha kuwa tamko la tarehe Machi 21 la kumtaka Prof Mwandosya kuwania urais halikutolewa na uongozi wa jumuiya kama watoa tamko hilo walivyobainisha.
Nyanga alisema waliotoa tamko hilo walikuwa watu wachache wasio na nia njema juu ya shirikisho,Chama na taifa kwa ujumla,
“Kimsingi tumesikitishwa sana na kuhuzunishwa sana juu ya matamko hayo ambayo yapo kinyume na misingi ya kimaadili ya chama cha mapinduzi licha ya ukweli kwamba watu hawa si viongozi wala hawakuwahi kuwa viongozi wa shirikisho la vyuo vikuu mkoa wa Mbeya.Tunashangazwa na matamko yasiyo na tija kwa shirikisho na kwa chama yaliyotolewa na watu ambao si viongozi wa shirikisho letu” alisema Nyanga.
Alisema msimamo wa shirikisho hilo ni kutofungamana na upande wowote wa urais kwa sasa wakiamini kwamba wakati muafaka ukifika vikao halali vya chama vitawaletea mgombea wa urais anayetosha kupeperusha bendera ya chama chao katika uchaguzi mkuu ujao.
Mnamo Machi 21 mwaka huu watu waliojiita viongozi wa shirikisho hilo mbelea ya wanahabari walitoa tamko la kumtaka Prof Mwandosya kuchukua fomu ya kuwania urais wakisema ana sifa za kuwania nafasi hiyo.
Akisoma tamko hilo Oscar Mwaihabi aliyejitambulisha kama katibu wa shirikisho alisema kwa pamoja wanashirikisho wamekubaliana kumshawishi Prof Mwandosya baada ya kuridhishwa na sifa alizo nazo.
Na Mbeya yetu 

0 comments: