Thursday, 2 October 2014

CHADEMA WAMTUHUMU KAMAANDA WA POLISI MOAWA MBEYA (RPC AHMED MSANGI,)



 Kulia ni Mwenyekiti wa (CHADEMA) MBEYA MJINI, John Mwambigija, akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa Mbeya Peack Hotel, kuhusu kusikitishwa kwa chama chake na kauli inayodaiwa kutolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, kuwa atakayeandamana atafanywa kitu mbaya, kamanda Msangi amekanusha kauli hiyo na kwamba hajawahi kusema kauli hiyo.
 Kulia ni Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi(CHADEMA), akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa Mbeya Peack Hotel, kuhusu kusikitishwa kwa chama chake na yeye binafsi na kauli inayodaiwa kutolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, kuwa atakayeandamana atafanywa kitu mbaya, kamanda Msangi amekanusha kauli hiyo na kwamba hajawahi kusema kauli hiyo.
 Kulia ni Mwenyekiti wa Vijana wa Chadem, wilaya ya Mbeya Mjini, Moses Mwaifunga.



CHAMA cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Mbeya mjini, kimesema kimesikitishwa na kauli inayodaiwa kutolewa hivi karibuni na Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, na kuandikwa katika gazeti moja la kiswahili linalotolewa kila siku nchini Tanzania, kuwa watakaothubutu kuandamana atawafanya kitu mbaya.

Wakizungumza na vyombo vya habari leo, katika ukumbi wa Mbeya Peack Hotel Jijini hapa, wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi(Sugu), walisema kuwa wanalaani kauli hiyo na kwamba anapaswa akanushe ndani ya siku tatu.

Mwenyekiti wa Chadema wa wilaya hiyo, John Mwambugija, amesema kuwa, hawakuandamana si kwa ajili ya kuogopa nguvu ya polisi, bali waliangalia mustakabali wa suala la usalama wa mji na wanawake.

“Vurugu zikitokea hapa, wanaoathirika ni wanawake na tuliona hakuna haja ya kufanya hivyo na kuharibu barabara kwasababu sisi ndiyo watawala na uchaguzi wa serikali za mitaa upo mbele yetu” alisema Mwambigija.

Huku akitamka maneno mengine makali na historia isiyo rasmi dhidi ya kamanda Msangi, Mwambigija alisema kwamba, kukaa kimya siyo uoga bali wameamua kutumia hekima na kama kamanda huyo hatoweza kukanusha kauli anayodaiwa kuitoa, watawaambia askari waliopo uraiani kuwa warejee makambin, maana wengi wao ni wafuasi wa chama hicho.

Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, alisema kuwa pamoja na kutokuwa na kawaida ya kuzungumza na vyombo vya habari, alilazimika kufanya hivyo jana kutokana na kauli inayodaiwa kutolewa na kiongozi huyo wa Polisi mkoani hapa, kwasababu yeye ni kiongozi mpenda amani.

“Hatuna shida na kamanda Msangi, lakini nimwambie kuwa oparesheni maalum ilimalizika Octoba 31, 2010, baada ya wananchi kumaliza uchaguzi na sasa kutokana na kauli hii, ajitathimini kuwa anataka rekodi gani” alisema Mbunge huyo huku akiwataja IGP Mwema, Suleiman Kova, Zelothe Steven kuwa historia ya utumishi wao ilitukuka kutoka Mbeya.


Alieleza kusikitishwa na kauli hiyo na kwamba kutokana na jambo hilo anamtangaza kamanda huyo kuwa adui nambari moja wa amani ya Mbeya na kumtaka waliomteua kumwamisha mkoani hapa.

Katika jambo hilo alisema ushauri anaoutoa kwa kamanda Msangi, ni kwamba “Hakuna utoto wa mjini katika kutimiza wajibu wa kazi” alisema Mbilinyi.

Naye Mwenyekiti wa Vijana wa chama hicho wilaya ya Mbeya Mjini, Moses Mwaifunga, alisema endapo kamanda Msangi atapuuza ushauri na maelekezo ya viongozi wake ya kukanusha kauli hiyo, vijana watafanya njama za ujasusi dhidi yake.

“Tutaingia mitaani mpaka ofisini kwake na ofisi ya Mkuu wa mkoa. Ni hatari kuongea haya, lakini tutalazimika kufanya ujasusi dhidi yake, maana naye anatengeneza ujasusi dhidi yetu” alisema Mwaifunga.

Kwa upande wake kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alisema kuwa hata yeye aliyaona maandishi kwenye gazeti, lakini hakusema jambo hilo na kwamba kutokana na nafasi aliyonayo hawezi kuyatamka hayo.

Alisema anawapa pole viongozi hao wa Chadema na wafuasi wao kutokana na usumbufu uliojitokeza kutokana na maandishi ya gazeti na kwamba tayari amewasiliana na waandishi husika na kuwaambia kuwa hawajatenda haki.

“Hata mimi niliyaona kwenye gazeti, sijatamka, nakumbuka alikuja huyo mwandishi na kuniuliza kuhusu maandamano ya Chadema, nilimwambia kuwa maandamano hayo ni batili na atakayekiuka atachukuliwa hatua za kisheria. Chadema ipo kisheria na tunawaheshimu nao wanatuheshimu” alisema kamanda Msangi.

Aliwaomba viongozi hao kuendeleza mshikamano na jeshi la polisi na yeye binafsi kwa ajili ya mustakabali wa amani na ustawi wa wananchi wote maana hata yeye ni mkazi wa Jimbo hilo na Mbilinyi ni Mbunge wake. 

Kwa hisani ya kalulunga media

0 comments: