Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, ACP Thobias Sedoyeka akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake.
Na Nathaniel Limu, Singida
POLISI mkoani Singida inamshikilia mwanamke mmoja kwa tuhuma ya kusababisha kifo cha mtoto wa mwaka mmoja na mama mtoto kulazwa baada ya kunywa pombe ya ‘Mtukuru’ nyumbani kwa mtuhumiwa.
Kamanda wa polisi mkoa, Thobias Sedoyeka alimtaja mwanamke anayeshikiliwa kuwa ni Anastazia Kadama (35) mkazi wa kijiji cha Msule, Misughaa wilayani Ikungi mkoani Singida.
Alisema kuwa tukio hilo ni la Jan 07 mwaka huu majira ya saa 3.15 asubuhi kijijini hapo.
Alisema kuwa siku ya tukio, mtuhumiwa Anastazia aliandaa pombe ya kienyeji iitwayo ‘Mtukuru’ kwa ajili ya kuwaalika majirani kwenda kumsaidia kulima shamba lake lakini kwa bahati mbaya siku hiyo mvua kubwa ilinyesha kiasi cha kuzuia shughuli hiyo kufanyika.
Kutokana na kuhofu pombe hiyo kuharibika, mtuhumiwa inadaiwa kuwa aliamua kuigawa kwa watu ili wainywe bure; mmoja wa watu hao akiwa mama wa mtoto aliyekufa, Magdalena Muna.
Alisema kuwa baada ya Magdalena kuionja pombe hiyo alimpa mtoto wake wa mwaka mmoja, Josephat Ntui, naye akanywa.
Kamanda Kamwela alisema kuwa baada ya Magdalena na mtoto wake kunywa pombe hiyo, walianza kutapika na kuharisha jambo lililosababisha wakimbizwe hospitali ya misheni Makiungu kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa mtoto huyo alizidiwa njiani kisha akafariki dunia kabla ya kufikishwa hospitalini lakini mama yake alifika akiwa hai na bado anaendelea na matibabu.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Kamwela amewataka wakazi wa mkoa huu kuwashirikisha wataalamu wa afya katika shughuli zao mbalimbali za kuchinja, kuandaa chakula au pombe za kienyeji ili kuepukana na matatizo yasiyo ya lazima.
0 comments:
Post a Comment