Nguza
Vicking 'Babu Seya' akiwa na mwanawe Johnson Nguza 'Papii Kocha'
wakiwa na nyuso za furaha wakati wakitoka katika Mahakama ya Rufaa baada
ya majaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania kusikiliza maombi yao ya
kuitaka mahakama hiyo kupitia hukumu iliyoitoa mwaka 2010. (Picha:
Francis Dande)
Wakili Mabere Marando, amedai Mahakama
ya Rufani, iliteleza kisheria katika uamuzi wake ambao uliwatia hatiani
na kuwahukumu kifungo cha maisha mwanamuziki Nguza Vikings au 'Babu
Seya' na mwanawe Johnson Nguza 'Papii Kocha'.
Marando alidai jana
mbele ya jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani lililotoa hukumu
hiyo, likiongozwa na Jaji Natharia Kimaro, kwamba mahakama iliteleza kwa
kutozingatia miongozo ya kisheria ya nanma ya kuchukua ushahidi wa
mtoto, kutoitwa kwa mashahidi muhimu. Mbali na Jaji Nathalia, Majaji wengine ni Mbarouk Mbarouk na Salum Massati.
Wakili
huyo, alidai hayo wakati wa kusikilizwa kwa maombi ya mapitio ya hukumu
hiyo, iliyotolewa Februari, 2010, Jopo hilo liliwatia hatiani Babu Seya
na mwanawe Papii na kuwapa adhabu ya kifungo cha maisha. Jopo hilo
liliwaachia huru watoto wengine wa Babu Seya, Nguza Mbangu na Francis
Nguza.
Marando alidai mahakama hiyo ilijiridhisha kulikuwa na
makosa katika kupokea ushahidi wa watoto na kwa sababu matakwa ya sheria
hayakufuatwa hivyo ushahidi huo ulipaswa kufutwa na waleta maombi
kuachiwa.
"Mlikubaliana na sisi kwamba Mahakama ya Kisutu
ilikosea haikuzingatia uchukuaji wa ushahidi lakini mlisema ilimradi
kuwe na ushahidi wa kuunga mkono. Sisi tulisema hapana,"alidai.
Pia,
alidai mahakama hiyo, ilikosea katika hukumu yake kwa kusema kuna
shahidi wa 13 aliyedai kwenye nyumba ya Babu Seya kuna mlango wa siri
ambao mtu anaweza kuingia na asionekane, ushahidi ambayo haupo na wala
shahidi huyo hakusema hivyo.
“Mashahidi walisema wao waliona
katika nyumba ya Babu Seya kuna milango miwili wa mbele na nyuma na yote
inainghia sebuleni, mtu huwezi kuingia katika chumba chochote bila
kupitia sebuleni... Sasa katika ukurasa wa 38 wa hukumu yenu, mmetamka
kwamba shahidi wa 13 aliiambia mahakama kuna mlango fulani wa kuingia
katika nyumba bila ya mtu mwingine kukuona. Ushahidi huo haupo katika
ushahidi wa shahidi wa 13 hawakusema. Haya ndiyo mambo
yanayojidhihirisha kuna kuteleza," alidai Marando.
Aidha, alidai
katika ushahidi wa mashahidi wanaohusika na ushahidi uliowatia hatiani
Babu Seya na Papii Kocha, walidai walikuwa wakiingia katika nyumba hiyo
wakitokea dukani kwa Mangi ambaye alikuwa akijua kinachotokea.
Marando
alidai kwa mujibu wa sheria, upande wa Jamhuri ulipaswa kumleta Mangi
ambaye ni shahidi muhimu ili aje kuthibitisha, lakini katika hukumu yao
walisema upande huo una hiari wa kumuita shahidi wanayemtaka, kauli
ambayo ni kinyume cha sheria.
Alidai kuna kijana anaitwa Size
ambaye anadaiwa alikuwa anawakusanya watoto wa kike na kuwapeleka kwa
Babu Seya na kufanya kinachodaiwa kutendeka, lakini hakuitwa na wala
mahakama hiyo katika hukumu haye haimkumzungumzia.
Hoja nyingine,
Marando anadai mahakama hiyo, iliteleza kwa kutotoa maoni yake juu ya
utetezi wao, kuhusu uwepo wa watu katika nyumba ya Babu Seya, ambao
walidai ingekuwa si rahisi watoto kuingia bila ya wao kuwaona kwa kuwa
kuna milango miwili ambayo inaingia sebuleni.
"Naomba mpitie tena
hukumu yenu na kurekebisha mambo ninayoona yana makosa ya kiuterezi na
mkikubaliana nasi mfute washitakiwa kutiwa hatiani na mfute adhabu zao,"
aliomba Marando.
Upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na
Wakili wa Serikali Mkuu, Jackson Bulashi, akishirikiana na Mawakili wa
Serikali Waandamizi, Mwangaza Mwipopo, Emmaculata Banzi, Joseph Pande na
Wakili wa Serikali Apimaki Mabrouk.
Wakili Bulashi aliiomba
mahakama hiyo, kutupilia mbali maombi hayo kwa sababu yalishatolewa
uamuzi katika rufani waliyokata waleta maombi. Alidai kwa upande wao
wanaona hakuna makosa yaliyofanywa katika kufikia uamuzi huo na kwamba
kilichowasilishwa ni sababu za rufani ambazo tayari zilishatolewa
uamuzi.
Jopo la Majaji lilisema kuwa limesikia hoja za pande zote
na kwamba wataarifiwa tarehe ya kutolewa uamuzi. Awali, jopo hilo
lilitupilia mbali maombi ya mapitio yaliyokuwa yamewasilishwa na Babu
Seya na Papii Kocha mwenyewe kwa msaada kutoka gerezani, kwa kuwa
hawakutumia vifungu sahihi kuyawasilisha.
Na
FURAHA OMARY, gazeti la Uhuru —
Nguza
Vicking na mwanaye Johnson Nguza katika chumba cha Mahakama ya Rufaa
Tanzania jijini Dar es Salaam leo, kabla ya kuanza kusikilizwa kwa rufaa
ya kesi yao. (Picha: Francis Dande)
MWANAMUKIZI
wa muziki wa dansi nchini Nguza Vicking ‘Babu Seya’ na mwanae Johnson
Nguza 'Papi Kocha Mtoto wa Mfalme', wameiomba Mahakama ya Rufaa nchini
iifanyie upya hukumu yake iliyoitoa Februali mwaka 2010 ambayo
iliwahukumu kifungo cha maisha kwasababu hukumu hiyo ina utetelezi wa
wazi wa kisheria.
Ombi hilo Na.5/2010 liliwasilishwa kwa niaba
yao na wakili wao Mabere Marando jana mbele ya jopo lilelile lilotoa
hukumu ya awali ya Februali 2010 ambalo linaongozwa na Jaji Nataria
Kimaro, Salum Massati na Mbarouk .S.Mbarouk.
Wakili Marando
alidai kwa mujibu wa kanuni ya 66 ya Mahakama ya Rufaa ya mwaka
2009 inatoa mamlaka kwa mahakama ya rufaa kufanya mapitio ya hukumu
inazozitoa hivyo wateja wake wamewasilisha ombi hilo la mapitio
kwasababu wanaamini mahakama yake ilikosea wazi wazi kisheria katika
hukumu yake ya Februali 2010 na kwa mujibu wa kanuni hiyo inatoa mamlaka
kwa mahakama hiyo kufanya mapitio ya hukumu yake.
Wakili
Marando alieleza kuwa ombi lake amelileta chini ya kifungu cha 3 aya A
ya Kanuni ya Mahakama ya Rufaa ya mwaka 2009 , ikisomwa pamoja na
Ibara 13 (3) (6)(a) ya Katiba ya nchi, litaja moja ya utelezi wa wazi
wazi wa kisheria uliofanywa na mahakama hiyo, ni kwamba katika hukumu
hiyo kuna baadhi ya aya inasomeka kuwa majaji hao walikubaliana na hoja
yake iliyodai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,
wakati inasikiliza kesi hiyo, ilikosoea kufuata utaratibu wa kurekodi
ushahidi wa watoto waliokuja kutoa ushahidi katika kesi hiyo na kwamba
mahakama ya rufaa ikasema licha ya taratibu za kurekodi ushahidi wa
watoto kukiukwa, mahakama yake iliona kuna ushahidi unaounga mkono na
kwamba mahakama ya rufaa ilitumia ushahidi wa kuunga mkono ndiyo
walioutumia kuwatia hatiani waomba rufaa kwa adhabu ya kifungo cha
maisha.
“Waheshimiwa majaji kwasababu jopo lenu katika hukumu
yake lilikiri wazi wazi kuwa mahakama ya kisutu ilikosoea kurekodi
ushahidi wa watoto wa dogo ambao walidai walitendewa vibaya na waomba
rufaa(Nguza na Papii), na sheria za nchi zipo wazi kabisa zina sema
endapo mahakama itabaini kuwa mahakama ya chini ilikiuka taratibu za
kurekodi ushahidi wa watoto wa dogo, basi ushahidi ule wa watoto wa dogo
uliotumika katika mahakama ya chini kuwatia hatiani washitakiwa,
ushahidi huo wa watoto unafutwa na waomba rufaa au washitakiwa
wanaachiriwa na pia maamuzi ya kesi mbalimbali yaliyokwisha kutolewa na
mahakama hii;
“Nafahamu ni kazi ngumu sana kuwashawishi nyie
majaji kubadili uamuzi wenu mlioutoa katika hukumu ya Februali 2010
ambapo mliwatia hatiani wateja wangu, ila kwa uterezi huo wa kisheria
niliouanisha unaonyesha katika hukumu yenu mlikubaliana na hoja yangu
kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kurekodi ushahidi watoto wadogo
,naamini mtatumia busara zenu na kufuata sheria inayosema wazi wazi kuwa
endapo utaratibu wa kurekodi ushahidi wa mtoto utakiukwa basi ushahidi
huo utafutwa na wateja wangu wataachiliwa huru, basi leo naiomba
mahakama hii iwaachirie huru wateja wangu’ alidai Marando.
Kwa
upande wao mawakili wa upande wa mjibu maombi (DPP),Angaza
Mwipopo,Jackson Mlati, Imaculata Banzi na Joseph Pande waliomba mahakama
hiyo itupilie mbali ombi hilo kwasababu sababu zote alizozitoa jana ni
sababu ambazo alizitoa wakati wa usikilizwaji wa rufaa na ziliamliwa
katika hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo Februali mwaka 2010.
Jackson
alidai kama Marando anaona hukumu ya mwaka 2010 ilikuwa na dosari ,
basi angeomba mahakama hiyo impangie jopo la majaji watano wa kusikiliza
ombi na siyo ombi lake kuja kusikilizwa na jopo la maji watatu wale
wale waliotoa hukumu ile ambayo Marando anadai ina dosari.
“Hoja
za Marando ni za kirufaa, na hoja zake zote anazotaka kuonyesha hukumu
ya mahakama hii ina dosari zilishaamriwa na mahakama hii wakati
ikisiliza rufaa ya wateja wake mwaka 2010 na tunamtaka Marando aelewe
kuwa hakuna maamuzi yasiyonamwisho hivyo sisi tunaomba ombi la Marando
linalotaka mahakama hii ifanyiwe mapitio hukumu yake halina
msingi”alidai wakili Jackson.
Aidha Jaji Kimaro alisema
amesikiliza hoja za pande zote mbili akaamuru waomba rufaa warejeshwe
gerezani na kwamba mahakama itatoa tarehe ya kutoa uamuzi wake kuhusu
maombi hayo kwa pande zote mbili.
Aliyekuwa Hakimu wa Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu Addy Lyamuya, aliyekuwa jaji wa Mahakama Kuu
Thomas Mihayo na jopo hilo la majaji wa tatu linaloundwa na Jaji Kimaro
,Massati na Mbarouk liliwatia hatiani kwa makosa ya kuwabaka watoto
wadogo na likawahukumu kifungo cha maisha gerezani na hadi sasa
wameishakaa gerezani kwa miaka kumi.
Mahakama ya Rufaa, Februali
mwaka 2010 ,ilirekebisha hukumu ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Kisutu
ambapo iliwaachiria huru waomba rufaa wawili katika kesi hiyo ambao ni
watoto wa Nguza Vicking, Nguza Mbangu na Francis Nguza waliachiwa huru,
huku Viking na Papi Kocha wakiendelea kutumikia kifungo chao hadi sasa.
Hata
hivyo jana mahakama hiyo ilifurika wanamuziki, mashabiki, ndugu wa
washitakiwa na wengine walilazimika kukaa sakafuni ambao walikuja
kusikiliza kesi hiyo.
Na HPPINESS KATABAZI, Tanzania Daima
Taarifa mbili zimepachikwa hapo chini kwa uchambuzi wako, kutoka magazeti ya UHURU na TANZANIA DAIMA